MJADALA WA LWAKATARE NA UGAIDI WAWASHA MOTO BUNGENI.

 
DODOMA-TANZANIA,
MKURUGENZI wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayekabiliwa na kesi ya ugaidi mahakamani, Wilfred Lwakatare, jana alilitikisa Bunge baada ya kuhusishwa katika mjadala.

Lwakatare alijadiliwa wakati wabunge walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Aliyeanzisha mjadala huo, ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), ambaye alianza kwa kuwatuhumu viongozi wa Chadema, wamekuwa wakipanga kuua watu na wakati huo huo wakitaka wananchi wawape ridhaa ya kuongoza nchi.

Alisema pamoja na viongozi hao kuwa na tabia hiyo, wamekuwa wa kwanza kulalamika juu ya vitendo vyao na kwamba tabia hiyo ni sawa na mchawi ambaye akiroga mtu na kumuua, anakuwa wa kwanza kulia akionyesha uchungu alionao juu ya marehemu.

“Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo limekuwa likiandikwa na kulalamikiwa na watu, kwamba ugaidi ugaidi. Katika jambo hili nawaomba Watanzania wasikilize kwa makini, kuna jambo lilitokea na jambo hili ni jambo la kigaidi, limeandikwa sana na kwa masikitiko linapotoshwa, yaani watu wanapotosha mpaka mambo yanayohusu maisha ya watu.

“Eti wanasema usalama wa taifa, mara wanasema polisi wanatesa watu, katika hili wala msihangaike na kwenye jambo hili hakuna polisi wala usalama wa taifa. Jambo la mkanda, aliyerekoki huo mkanda yuko tayari kusema kokote, aliyeniletea huo mkanda yuko tayari kusema kokote na mimi niko tayari kwenda kokote hata kama ni mbinguni.

“Chadema walipanga kuteka na kuua na huyu mwandishi walipanga kumuua eti wanadai picha ilitengenezwa, sasa kwa taarifa yenu hata pale alipokuwa anaongea, (akimaanisha Lwakatare), aliandika hata ile karatasi ninayo, ni hii hapa, fingerprint ni ya kwake, mwandiko ni wa kwake na vyote alivyokuwa anafanyia kazi vimepatikana na alisema atatoa ushahidi na mimi niko tayari kutoa ushahidi kokote iwe ni hapa na hata mbinguni nitakwenda,” alisema Mwigulu akionyesha karatasi hiyo na kuongeza.

“Eti Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), anasema anayewasiliana na gaidi eti naye aunganishwe na ugaidi, hebu fikirieni, yule aliyekuwa akipanga njama ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, kama ni viongozi, amewasiliana na viongozi gani kama siyo wakubwa zake ambao wamemwagiza kufanya hayo tena?

“Jitihada zinazoonyeshwa ambazo ni za kumtetea mtu hata kabla hajafika mahakamani, inadhihirisha ule ulikuwa ni mpango wa chama.

“Kwa kauli hii, ambayo ameandika kiongozi wa upinzani, viongozi wanaowasiliana nao waunganishwe katika kesi ya ugaidi kuanzia leo wakamatwe na polisi, hapa simuoni kiongozi wa Kambi ya Upinzani, labda wameshamkamata,” alisema Mwigulu.

Katika mazungumzo yake, Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alitaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, akamatwe kwa kuwa alihusika kumtetea Lwakatare.

Kwa mujibu wa Mwigulu, aliyekuwa akipanga njama za ugaidi huo ni mwanachama wa Chadema na kwamba fedha zilizotumika katika kufanikisha mpango huo, ni za chama hicho.

“Mnasubiri nini polisi, mtu ameshaomba kuunganishwa mwenyewe katika kesi?”

“Mkishapanga maovu mnawahi kwenda kutetea kama vile mchawi ambaye akishaua, anawahi kwenda kulia na kugalagala msibani. Mimi kwenye hili suala la mauaji, nawaomba Chadema mfanye vitu viwili, kwanza kimbieni haraka zaidi kwenye makanisa ama misikiti mliyokaribu nayo ili mkatubu kuwa mmepanga kuwauwa watu wasio na hatia.

“Baada ya kuomba toba, mrudi kutubu kwa wananchi, yaani mnataka uongozi halafu unawaza kuuwa watu, look at you,” alisema.

Wakati akiendelea kusema, Mbunge wa Mbulu, Mustafa Akunay (CHADEMA), aliomba utaratibu na kumlalamikia Mwigulu, kwamba anazungumzia masuala ya Lwakatare wakati akijua yako mahakamani.

Alipomaliza kusema hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alikubaliana naye na kuwataka wabunge waheshimu kanuni za Bunge. Hata hivyo hoja hiyo Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Pauline Gekul alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 68 (7).

Alipokuwa akizungumza, alionyesha kutoridhishwa na maelezo ya Spika kwa kuhoji kama wabunge wanatakiwa kufuata kanuni kwa nini Mwigulu alipokuwa akizungumzia masuala yaliyo mahakamani hakuzuiwa na badala yake aliachwa na kuendelea kusema hadi mwisho.

Hoja hiyo, ilimfanya Spika asimame tena na kusema wabunge wanatakiwa kufuata kanuni kwa kuwa hata Mbowe alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi yake juzi kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna maneno yasiyofaa aliyasema, lakini akaachwa hadi mwisho.(MTANZANIA)

0 comments: