MIAKA 29 BAADA YA KIFO CHA EDWARD SOKOINE-HISTORIA,NUKUU NA PICHA

Hayati  Edward Moringe Sokoine


Edward Moringe Sokoine (1938 - 12 Aprili 1984) alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa awamu mbili, tangu tarehe 13 Februari 1977 hadi 7 Novemba 1980, na tangu tarehe 24 Februari 1983 hadi kifo chake, alipofariki kutokana na ajali ya gari. 

Uongozi wake ulionekana kuwa wa mfano kwa jinsi alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi huku akikemea ulaji rushwa na ubadhirifu wa mali za umma. 

Sokoine alifariki kwa ajali ya gari wakati akitoka kwenye kikao cha bunge Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Wengi wanashuku ajali hiyo kuwa ilipangwa, ingawa mpaka leo bado ni kiza kitupu.

Kifo chake kilileta majonzi makubwa kwa Watanzania wa kawaida ambao walikuwa wanamtarajia kuwatetea wanyonge na kuinua hali ya maisha yao. 
 
Mwili wa Edward Moringe Sokoine ulizikwa nyumbani kwao Monduli, mkoani Arusha.
Leo Tanzania inaazimisha miaka 29 tangu kufariki kwa ndugu Edward Moringe Sokoine (01/08/1938-12/04/1984)   Waziri Mkuu wa aina yake nchini Tanzania.Sokoine aliongoza katika kipindi ambacho nchi ilikuwa katika hali ngumu sana ya kiuchumi. 
Hayati Sokoine na Mwalimu Nyerere.
Zifuatazo ni nukuu muhimu za shujaa huyo kutoka katika Kitabu cha Edward Moringe Sokoine: Kiongozi wa Watu Aliyejitolea kilichoandikwa na Luteni Kanali Albert N. Kigadye mnamo mwaka 1984:


"Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake. Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu" - Edward Moringe Sokoine, 26 Machi 1983

"Juu ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa kupunguza uongezaji wa wataalam wasiohitajika katika Serikali na katika mashirika ya umma mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali nzuri" - Edward Moringe Sokoine, 23 Oktoba 1982
Gari la Hayati sokoine baada ya ajali.
"Serikali inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka itasimamia bei ya mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine ni lazima vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha" - Edward Moringe Sokoine, 24 Septemba 1983

"Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe. Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa" - Edward Moringe Sokoine, 4 Oktoba 1983

"Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka thelathini hadi arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae, 'mali hii umeipata wapi?'" - Edward Moringe Sokoine, 23 Oktoba 1983

"Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio wengi" - Edward Moringe Sokoine, 1Februari 1977

0 comments: