Rais Obama awasili, aisifu Tanzania



Dar es Salaam. Rais Barack wa Marekani, Obama ametaja vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania, ambavyo vinajumuisha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Kiongozi huyo aliwasili Dar es Salaam jana mchana ikiwa ni nchi ya mwisho katika ziara yake barani Afrika ikitanguliwa na Senegal na Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Rais Obama alisema aliainisha mambo hayo wakati alipozungumza na mwenyeji wake huyo.
Alisema katika mazungumzo hayo, waligusia mradi wa mkubwa wa umeme uitwao Power Afrika wenye lengo la kuongeza kiwango cha umeme kinachozalishwa nchini na barani Afrika ili kupata umeme nafuu na wa uhakika utakaochagiza kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Nchi nyingine za Afrika ambazo zitanufaika na mpango huo ni Kenya, Ghana, Liberia, Nigeria na Ethiopia.
Rais Obama alisema pia wamezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ukuzaji wa demokrasia na utawala bora. Alimzungumzia pia mchezaji nyota wa mpira wa kikapu wa Tanzania, Hashimu Thabeet anayecheza katika Ligi Kuu ya Marekani (NBA), akiwa na timu ya Oklahoma Thunder ya Marekani, akisema hawakuzungumzia suala lake na kuahidi kufanya hivyo siku nyingine.
Akijibu swali iwapo anaridhishwa na misaada ambayo nchi yake inatoa kwa Tanzania, Rais Obama alisema anafarijika kwa matunda yanayopatikana katika mapambano dhidi ya malaria, barabara mpya zinazojengwa na katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Hatutoi dawa, bali tunajenga miundombinu ya afya, hatutoi chakula, bali kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula pia tunasisitiza kubadilishwa kwa sheria mbalimbali ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kuleta mitaji yao kwa wingi zaidi, lakini jambo la muhimu ni kuijenga Afrika,” alisema.
Kuhusu sekta ya utalii, Rais Obama alisema watatangaza vivutio vya Tanzania, lakini kwa kuwa ameambiwa ujangili ni tatizo, Serikali yake itaisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tutatangaza utalii, nimeelezwa ujangili ni tatizo hivyo Marekani itasaidia kupambana na changamoto hiyo na tutaongeza fedha kuhakikisha hali hiyo inatokomea,” alisema.
Akichangia hoja ya misaada ya Marekani, Rais Kikwete alisema Mradi wa Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC), umekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.
Alisema kupitia MCC, Tanzania imepata msaada wa kujengewa barabara katika maeneo ya vijijini na yale yanayozalisha chakula kwa wingi.(MWANANCHI)

0 comments: