PILIKA PILIKA NYUMBANI KWA MANDELA ZAONGEZA HOFU.
Johannesburg, Wakati kukiwa na vita ya chini kwa chini dhidi ya vyombo vya habari vinavyofuatilia mwenendo wa afya ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kumekuwa na pilika nyingi katika makazi ya kiongozi huyo yaliyopo eneo la Houghton, Mtaa wa Laan 12, jijini Johannesburg.
Leo ni siku ya 22 tangu Mandela alazwe katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliopo Pretoria akiugua ugonjwa wa figo na katika siku saba zilizopota taarifa rasmi zinasema “hali yake ni mbaya”.
Usiku wa kuamkia jana, Mwenyekiti wa taifa wa chama tawala cha ANC, Baleka Mbete aliongoza maombi ya kumwombea Mandela kwa wanachama na makada wake waliopo majimbo ya Cape Town na Eastern Cape huku akisisitiza:
“lazima wananchi wa Afrika Kusini, wafike mahali wamruhusu Mandela ampumzike kwa mapenzi ya Mungu”.
Wakati hayo yakiendelea pilika katika makazi ya Mandela ziliwahusisha makundi ya watu na kampuni kadhaa za jijini Johannesburg, wakiwamo watu waliokuwa wakifanya usafi.
Kazi hiyo ilifanyika kwa kufagia na kuzoa taka, usafi wa vitalu na kubadilisha mawe, utengenezaji wa bustani za maua na pia mafundi waliokuwa wakifanya shughuli za marekebisho ya njia za umeme katika eneo hilo.
Mmoja wa majirani katika eneo hilo alyejitambulisha kwa jina la Jacob Brews alisema: “Huwa watu wanafanya usafi hapa lakini ninaona kama leo kuna jambo la ziada hapa. Maana watu ni wengi na kila mmoja anaonekana anatekeleza wajibu wake”.
Katika nyumba hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya magari kuliko kawaida na ilipotimu saa 6.00 mchana magari saba yalikuwa yameegeshwa mbele ya lango la nyumba hiyo ikiwa ni ishara kwamba wahusika wake walikuwa ndani.
Mwananchi lilishuhudia magari mengine yakiingia ndani na kutoka kila baada ya muda, huku baadhi ya wageni wakiingia ndani wakiwa wamebeba maua. Kabla ya jana hakukuwa na watu wengi walioonekana wakiingia katika nyumba hiyo.
Watu wanaodhaniwa ni maofisa usalama pia walikuwa wametapakaa nje ya makazi hayo walikuwa wakifuatilia kwa karibu mazungumzo ya waandishi wa habari na walinzi pamoja na watu waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali.
Mmoja wa walinzi hao aliliambia Mwananchi kuwa hawezi kuzungumza chochote. “Tunafuatiliwa sana maana hawataki tuzungumze chochote kile ambacho kinatokea huko ndani, labda kama ungenitafuta nje ya hapa”.
0 comments: