KUNDI LA LRA LADAIWA KUTEKELEZA MAUAJI YA WATU TAKRIBNI LAKI MOJA.


 

DRC CONGO,Ripoti ya Umoja wa Mataifa imearifu kwamba kundi la waasi la Lord Resistence Army (LRA) linaloongozwa na Joseph Kony anayetafutwa kwa udi na uvumba na mahakama ya kimataIfa ya uhalifu wa kivita ya ICC pamoja na Marekani, limetekeleza mauaji ya watu takriban laki moja katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, na kuwateka watoto wapatao sitini.

Ofisi ya haki za binadamu kwenye Umoja huo inayoongozwa na Navi Pilley imeendesha uchughuzi kuhusu uhalifu uliotekelezwa na kundi hilo tangu mwaka 1987 na inataraji kuweka hadharani ripoti hiyo hivi karibuni.

Kundi hilo la LRA linatuhumiwa pia kuwatekea nyara watoto wadogo wapatao elfu sitini na kuwashirikisha katika uhalifu, lakini pia kusababisha watu milioni mbili na nusu kutoroka makwao, imeendelea kusema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Kundi la LRA linatambulika kuwa kundi baya zaidi la uasi katika ukanda wa Afrika Mashriki na kati, lilikuwa liendesha harakati zake kaskazini mwa Uganda mwaka 1988, na baadae wapiganaji wake walielekea huko kaskazini mwa DRCongo na wengine nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati huku wengine wakielekea Sudani na Sudani Kusini

waasi hao wanatambulika kutokana na vitendo vya uporaji, ubakaji, mauaji na kuwaajiri watoto wadogo katika kundi hilo na kuwashirikisha katika vitendo mbalimbali vya uhalifu kama vile kuwafanya mateka wa ngono.

Jeshi la Uganda likisaidiwa na mamia ya wanajeshi wa Marekani linaendesha tangu mwaka 2008 operesheni ya kumsaka kiongozi wa waasi wa kundi hilo Joseph Kony anaesadikiwa kujificha nchini Sudani kwa kusaidiwa na baadhi ya wanajeshi wa serikali ya Omar Hassan Al Bashir, duru za shirika la Marekani la "Resolve LRA crisis initiative".

Serikali ya Marekani ilitangaza kitita cha dola milioni tano kwa mtu yeyote atakaye toa taarifa za kumfichua kiongozi huyo anayetuhumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Licha ya kwamba mashambulizi ya kundi hilo la LRA, yamepungua kwa kiasi kikubwa, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anaona kuwa wapiganaji hao bado ni tishio kubwa katika maeneo ya mpakani baina ya DRCongo na Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa umesema kwamba kundi la LRA limetekeleza mashambulizi takriban 212 katika mwaka 2012 yaliosababisha vifo vya watu 45 na ambapo watu 220 walitekwa nyara na ambapo thuluthi moja ni watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka 18.

0 comments: