CAG ABAINI UBADHILIFU MKUBWA SERIKALINI.
DODOMA-TANZANIA,
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitolewa jana ikiweka bayana madudu mbalimbali ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, udhaifu katika usimamizi wa mikataba na Serikali kushindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Moja ya matatizo yaliyojitokeza ni Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya nyongeza ya mrabaha wa madini baada ya kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi nne.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2012, CAG Ludovick Utouh alisema pamoja na kuwapo mafanikio ya kimahesabu ukilinganisha na miaka iliyopita, bado kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.
Alilishauri Bunge kuangalia upya suala la kuivunja Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na mkakati wa ofisi kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kuangalia uhalali wake.
Hata hivyo, Utouh alikataa katakata kuzungumzia deni la taifa ambalo pia limeongezeka akisema “amefanya hivyo makusudi”.
Bajeti na miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa CAG, imebainika kuwa kuna tatizo kubwa la Serikali kushindwa kutoa kwa halmashauri mbalimbali fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge.
Alisema Bunge lilipitisha vifungu vya fedha za maendeleo vyenye jumla ya Sh595,064,422,505 katika halmashauri 113, lakini fedha zilizopokewa ni Sh345,568,067,477 sawa na asilimia 42 tu, hivyo kufanya upungufu wa Sh249,496,355,027.
Licha ya fedha hizo kutokutolewa zote, kiwango kilichotolewa hakikutumika chote kutokana na kucheleweshwa. “Hadi mwishoni mwa mwaka, kulikuwa na baki ya fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha Sh188,405,740,589 ambayo ni sawa na asilimia 55 ya fedha zilizotolewa na Serikali,” alisema Otouh na kuongeza: “Tunashauri bajeti iendane na shughuli zilizopangwa, kwa sasa utaratibu wa bajeti haujawa mzuri.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa kwa wabunge hazikutumika zote. Sh2,561,882,820 zilizotengwa kwa ajili ya sampuli ya majimbo 69 zilibaki.
“Sababu ya kutokutumika ni ama halmashauri hazina utaratibu maalumu wa kutumia fedha hizo au Serikali kutoa fedha hizo mwishoni mwa mwaka,” alisema.
Udhaifu katika usimamizi wa mikataba ya madini
Katika ripoti hiyo, CAG alisema Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa kukusanya Dola za Marekani 12,634,354 (sawa na Sh19,709,593,191) zilizotokana na ongezeko la mirabaha ya madini, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini.
Katika iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yake ya mwaka 2010/11 yanayofikia Sh253 bilioni yamelipwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara mwaka uliofuata wa 2011/12.
Katika kipindi hicho, CAG alisema dhamana za Serikali za jumla ya Sh578.4 bilioni zilikuwa zimeisha muda wake na hivyo kuifanya Serikali ikiwa mdhamini kuwajibika kulipa deni hilo.
Vilevile, CAG ameona kuna kodi inayopotea kutoka sekta isiyo rasmi, hivyo kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatumia vizuri makatibu kata kuwatambua walipakodi kama vile wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.(MWANANCHI)
0 comments: