UHABA WA MADAKTARI BINGWA WAIKUMBA MUHIMBILI
DAR ES SALAAM-TANZANIA,
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inakabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa wa upasuaji, hususan katika kitengo cha watoto wanaougua maradhi ya saratani (cancer surgeons).
Upungufu huo unaelezwa umetokana na baadhi ya madaktari bingwa waliokuwapo awali kufariki dunia mwaka jana, baadhi kuacha kazi na wengine kustaafu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini madaktari bingwa wawili walifariki dunia mwaka jana, ambao ni Dk. Enock Sayi na Dk. Profesa Primo Carneiro, wakati Dk. Catherine Mng’ong’o anaelezwa kuacha kazi, huku Dk. Petronella Ngiloi akistaafu kwa mujibu wa sheria.
Habari zilizopatikana hospitalini hapo na kuthibitishwa na mamlaka husika, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinasema mbali na hospitali hiyo Kuu ya Taifa kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa, inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa mashine za oksijeni za kisasa za ukutani.
Mashine za oksijeni zilizopo zinadaiwa kufanya kazi chini ya kiwango kinachotakiwa.
Lakini msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, pamoja na kukiri kuwapo kwa upungufu huo wa madaktari bingwa, amesema hilo haliwezi kuathiri shughuli za tiba katika kitengo hicho cha magonjwa ya watoto.
Aidha, anasema hospitali hiyo imesheheni vifaa vya kisasa, zikiwamo mashine hizo za oksijeni, zinazotumika kumsaidia mgonjwa kupumua.
Uchuguzi uliofanywa na gazeti hili katika Jengo la Watoto na kwenye baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini pia kuwapo kwa vichwa vya mashine za mitungi ya oksijeni vikiwa vimezungushiwa plasta kuzuia uvujaji hovyo wa hewa hiyo, hali inayohatarisha afya za wagonjwa wanaolazwa katika wodi zenye mashine hizo.
“Hayo mambo yanashughulikiwa na Bodi ya Muhimbili pamoja na Mkurugenzi wake. Kama masuala hayo unayouliza yatahitajika kufika wizarani, ndipo hapo na sisi tunaweza kutolea ufafanuzi, lakini ninavyojua Muhimbili kuna vifaa vyote vya kisasa na ndiyo maana imeitwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Mwamwaja.
Mmoja wa madaktari bingwa wa Muhimbili, ameliambia gazeti hili kwamba tangu walipofariki madaktari bingwa wenzake; Dk. Sayi na Profesa Carneiro mwaka jana, nafasi zao hadi sasa hazijajazwa.
Aidha, daktari bingwa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa sababu zilizo wazi kabisa, amethibitisha kuwapo kwa tatizo la madaktari bingwa katika kitengo cha saratani, baada ya Dk. Ngiloi kustaafu.
Alisema awali baada ya Dk. Ngiloi kustaafu, Dk. aliyechukua nafasi yake hiyo katika kitengo hicho alikuwa Dk. Mng’ong’o, lakini kwa sasa anadaiwa kuacha kazi hospitalini hapo.
0 comments: