TAIFA STARS KUPAMBANA NA ETHIOPIA LEO

    
  
ADDIS ABABA-ETHIOPIA,  Mechi ya kirafiki ya kimataifa baina ya timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) na wenyeji Ethiopia itapigwa kuanzia saa 11:30 jioni, taarifa ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ilisema jana.

Stars itashuka dimbani leo ikiwa na lengo la kujiongezea heshima kwa kuendeleza kichapo dhidi ya wenyeji ambao wamefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2013) zitakazoanza Janauri 19 nchini Afrika Kusini; ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kupata ushindi usiotarajiwa wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia "Chipolopolo" katika mechi yao nyingine ya kirafiki iliyochezwa Desemba 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja wa Addis Ababa uliopo katika mji huo mkuu wa Ethiopia.

"Mechi itachezwa kesho (leo) Addis Ababa Stadium kuanzia saa 11.30 jioni (Tanzania na Ethiopia hatupishani saa)," taarifa hiyo ilisema.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa timu iliwasili salama na kufikia katika hoteli ya Hilton na kwamba ilitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa kwa saa moja jana kuanzia saa 11.30 jioni.

Katika mechi yao iliyopita dhidi ya Zambia, goli pekee la Stars lililofungwa na Mrisho Ngassa lilitosha kuwashangaza nyota wakubwa wa Chipolopolo, akiwamo nahodha Christopher Katongo ambaye alikuwa ndiyo kwanza ametokea kushinda tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika 2012.

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na Ethiopia kutaka kupima nafasi yao kuelekea kwenye fainali za Mataifa ya Afrika huku Stars ikiitumia kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi 22.
Tanzania yenye pointi tatu inashika nafasi ya pili katika Kundi C la kuwania kufuzu kwa safari ya Brazil nyuma ya vinara Ivory Coast wenye pointi nne baada ya mechi mbili. Morocco ni ya tatu ikiwa na pointi mbili wakati Gambia inashika mkia ikiwa na pointi 1. Timu moja tu katika kila kundi (makundi 10) ndiyo inayosonga mbele kwa hatua inayofuata ya mechi za mtoano. Timu tano zitaenda Brazil.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema baada ya mechi hiyo, Stars inatarajia kucheza mechi nyingine angalau moja ya kimataifa kabla ya kuwavaa Morocco.

Wachezaji waliopo katika kambi ya Stars kwa ajili ya mechi ya leo ni pamoja na nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam FC), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), na Shomari Kapombe (Simba).

Wengine ni Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu  (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ) na Mrisho Ngasa (Simba)
.

0 comments: